Maisha, Huduma Na Urithi wa Derek Prince

Derek Prince alikuwa mwalimu wa Biblia aliyejulikana na kuheshimika sana kwa ufasaha wa theolojia na uthabiti kwa Imani ya Kikristo. Ni mwandishi wa vitabu zaidi ya 100 ambavyo vimeendelea kuvutia maelfu ya wasomaji kila mwaka.

Derek Prince

Huduma:
Mwalimu wa Kimataifa wa Biblia, mwandishi, mchungaji, mmishonari na mwanatheolojia.
Kuzaliwa
14 Agosti 1915, Bangalore, India
Kufariki
24 Septemba 2003 (miaka 88)

Yaliyomo

Bonyeza kwenda mahali husika

Maisha ya Awali

Derek Prince alizaliwa katika familia ya kijeshi huko Bangalore, India, mwaka 1915. Akiwa na umri wa miaka 14 alishinda ufadhili na kujiunga na Chuo cha Eton ambapo alisomea Kiyunani na Kirumi. Aliendelea na elimu ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza ,ambapo alihitimu kwa ufanisi juu ya Falsafa ya Kale na Kisasa kutunukiwa Uandamizi kwenye chuo kiitwacho King's College. Zaidi ya hayo, Derek alisoma lugha kadhaa za Kisasa ikiwa ni pamoja na Kiebrania na Kiaramaiki alipokuwa Chuo Kikuu cha Cambridge, na baadaye alijinoa zaidi kwenye Chuo Kikuu Cha Kiebrania mjini Yerusalemu.

Ingawa Derek alikulia kwenye Kanisa la Anglikana, aliacha mizizi hiyo alipokuwa Chuo Kikuu cha Cambridge na kuingia kwenye ulimwengu wa kutoamini uwepo wa Mungu. Na alipokuwa akitafakari miaka yake hiyo, alinukuliwa akisema:

Nilijua misemo na maneno marefu, na nilijaribu vitu vingi. Lakini, nikitazama nyuma, ninakiri kuwa nilikuwa nimechanganyikiwa na kufadhaika, nilivunjika moyo na kuanguka, sikujua wapi nitapata majibu

Vita Ya Pili Ya Dunia

Maisha ya Derek kitaaluma yaliingiliwa mwanzoni mwa Vita Ya Pili Ya Dunia. Mwaka 1940 aliandikishwa kwenye Jeshi la Kifalme Askari Wauguzi kama askari-asiyepigana kutokana na imani yake. Na kwa ajili ya kuendeleza taaluma yake atakapokuwa kwenye utumishi wa jeshi, Derek alichukua Biblia, ambayo wakati huo aliichukulia kama kitabu kwa kazi ya falsafa badala ya kuwa ni Neno lenye pumzi ya Mungu.

Mnamo tarehe 31 Julai 1941, alipokuwa kwenye kambi ya mafunzo ya Scarborough, Yorkshire, alikutana na nguvu za Yesu ambazo zilibadilisha mustakabali wa maisha yake. Akisimulia juu ya tukio hilo alisema:

Nilisikia sauti ya Yesu, ikisema wazi wazi kwa kupitia maandiko, Biblia. Na kutoka siku hiyo nilipoisikia sauti Yake, hadi leo, kuna vitu viwili ambavyo sina shaka navyo. Sijawahi  kuwa na shaka kwamba Yesu yu hai, na sijawahi kuwa na shaka kwamba Biblia ni Neno la Mungu

Hivyo ilianza safari ya kiroho kama mmoja wa walimu mashuhuri wa Biblia wa karne ya 20.

Muda mfupi baada ya kuongoka, Derek alihamishiwa Afrika Kaskazini kwa majukumu ya kijeshi jangwani kama askari muuguzi, na alibakia huko kwa utumishi huo miaka mitatu. Alitumia muda wake wa ziada kusoma Biblia na kuendeleza uhusiano wake na Mungu.

Baada ya kumalizika kwa vita, Derek aliondolewa jeshini wakati alipokuwa mjini Yerusalemu, aliposhuhudia utimilifu wa unabii wa kibiblia wa kurudi kwa Wayahudi katika Israel.

Lidia Prince

Mwaka 1946, Derek alimuoa mke wake wa kwanza, Lidia Christensen, mmishonari kutoka Denmark ambaye alikuwa anaendesha kituo cha watoto karibu na Yerusalemu. Kwa maana hiyo akawa baba wa kuasili wa binti wanane.

Derek na Lidia waliishi Yerusalemu mpaka wakati taifa la Israeli lilipoanzishwa mwaka1948. Walijikuta katikati ya mapigano baina ya vikosi vya Waarabu na Waisraeli wakati wa vita ya Uhuru, na kwa shingo upande walihamishwa kutoka nyumbani kwao mpaka Uingereza. Waliishi katikati ya mji wa London, ndipo Derek alipoanza kuhubiri kwenye eneo linalojulikana kama Speaker's Corner huko Hyden Park, ambapo mara nyingi aliandamana na Lidia na baadhi ya binti zao. Mara nyingine aliwaalika wahudhuriaji nyumbani kwake kwa ajili ya huduma zaidi, na hapo lilizaliwa kanisa. Hili liliendelea hadi mwaka 1956 wakati Derek na familia yake walipoitikia wito wa Mungu wa kwenda Kenya kama wamishonari mnamo Januari 1957.

Miaka iliyofuata, Derek na Lidia waliona matunda mengi ya huduma yao kwa wenyeji, ikiwa ni pamoja na binti mmoja aliyefufuliwa toka wafu kwa njia ya maombi.

Kufikia Mwaka 1962, wenzi hao walikuwa wameasili mtoto mchanga Mkenya aliyekuwa yatima kisha wakaenda kwenye likizo nchini Kanada. Lidia, aliyekuwa mkubwa kiumri miaka 25 zaidi ya Derek, alikuwa mwanzoni mwa umri wa miaka sabini na alitamani kuishi karibu na marafiki na waumini wengine. Akichochewa na uhitaji huo, Derek alikubali mwaliko wa kuwa mwalimu wa Biblia kwenye kanisa la Pentekoste huko Minneapolis.

Derek na Lidia Prince

Hata hivyo, kabla ya mwisho wa muongo, akina Prince walihama mara tatu zaidi; Seattle, Chicago na Fort lauderdale, mfululizo. Maendeleo katika huduma yalifungua milango mipya isiyotarajiwa, lakini wenzi hao walibaki waaminifu kwa wito hai wa Mungu ndani yao.

Kufikia mwaka 1968, huduma ya kufundisha ya Derek iliongezeka kwa kasi kupitia vuguvugu lilioibuka la Karismatiki. Alisafiri sana, akihubiri Neno kwa nguvu na mamlaka.

Mnamo Oktoba 5 mwaka 1975, Lidia Prince alifariki kwa amani akiwa na umri wa miaka 85, akiwa amezungukwa na familia yake. Yeye ni mwandishi wa "Appointment in Jerusalem (Miadi Huko Yerusalem), ambacho kilichapishwa muda mfupi kabla ya kifo chake mwaka huo huo.

Ruth Prince

Mnamo mwaka 1978, Derek alioa mke wake wa pili, Ruth Baker, Mmarekani asiyekuwa na mwenzi, aliyekuwa mama wa watoto watatu wa kuasili. Walikutana Yerusalemu wakati Derek alipotembelea Israeli akiwa na marafiki.

Kwa pamoja, awamu mpya ya huduma iliibuka kwa uzinduzi wa kipindi cha redio kiitwacho "Leo na Derek Prince." Hapo awali kilitangazwa katika vituo nane vya redio, idadi ya wasikilizaji iliongezeka na kukua kwa kasi na umaarufu wake kuimarika. Rekodi za mafundisho hayo leo hii zimesambazwa ulimwenguni na zinapatikana katika lugha mbali mbali.

Maelezo zaid juu ya upendo wa Derek na Ruth, yameandikwa kwenye kitabu cha "God is a Matchmaker" (Mungu ni Mshenga), ambacho waliandika kwa pamoja mwaka 1986.

Derek na Ruth Prince wakiwa katika picha ya pamoja kando ya Mto Zambezi, Zambia, mwaka 1985.

Ruth aliaga dunia huko Yerusalem mnamo tarehe 29 Desemba 1998 kutokana na kuugua muda mfupi, hata hivyo aina ya maradhi yake haikujulikana mara moja. Alikuwa na umri wa miaka 68 na alikuwa amehudumu na Derek kwa uaminifu kwa kwa zaidi ya miaka ishirini.

Kuzidiwa na huzuni, moyo wa Derek ulianza kujaa kisima cha uchungu. Alihisi nguvu chafu ambazo hatimaye zingemtenga mbali na Mungu, hivyo alitoa tamko hadharani wakati wa mazishi ya Ruth ambalo lilitabainisha miaka iliyobaki ya maisha yake. Wakati jeneza lilipokuwa linashushwa Derek alimshukuru Mungu kwa yote aliyoyafanya katika maisha ya Ruth, kwa dhati akithibitisha upendo na tegemeo lake kwa Baba yake wa mbinguni. akitafakari juu ya tukio hilo, baadaye alisema:

Ilikuwa wakati muhimu katika maisha yangu. Nilijua nisingeweza kuendelea mbele na maombolezo niliyohisi juu ya Ruth. Ningemlaumu Mungu kila wakati na hivyo mlango wa maisha yangu ungefungwa. Njia hii ndiyo pekee ingenifanya niweze kusonga mbele

Kifo

Derek Prince alifariki kifo cha kawaida mnamo tarehe 24 Septemba 2003, akiwa na umri wa miaka 88. Aliugua kwa muda mrefu na afya yake kudhoofika na alifariki usingizini nyyumbani kwake huko Yerusalem.

Alizikwa kwenye makaburi ya Kanisa la Alliance International huko Yerusalemu, jiwe kaburini mwa Derek linasomeka hivi:

DEREK PRINCE
1915 - 2003
AMEKWENDA NYUMBANI
Mwalimu wa Maandiko
Katika Kweli na Imani na Upendo
Ulio katika Kristo Yesu kwa Ajili ya Wengi
Mungu ni Mwaminifu

Derek Prince akihubiri katika Kanisa la Utatu (sasa Kanisa la Jiwe la Pembeni) huko San Antonio, Texas, mwaka 1974.

Mwalimu wa Biblia

Mwaka 1944, akiwa kwenye bohari ya ugavi wa vifaa tiba huko Kiriat Motzkin, Israel, Bwana alizungumza na Derek wazi wazi akisema:

Umeitwa kuwa mwalimu wa Maandiko katika kweli na imani na upendo ulio katika Kristo Yesu - kwa ajili ya wengi.

Ilionekana haiyumkiniki kutokana na kituo alichokuwepo, lakini baada ya muda yalitimilika sawa sawa na Mungu alivyoahidi mwaka 1941.

Itakuwa kama vile kijito kidogo. Nacho kijito kitakuwa mto. Na mto utakuwa mto mkubwa. Na mto mkubwa utakuwa kama ziwa. Na ziwa litakuwa kama bahari kuu, na itatokea kupitia wewe. Lakini kwa namna gani, si juu yako kujua, wewe hutajua ni kwa vipi, hutajua

Hadi leo, jina Derek Prince limebaki kama theolojia nzuri na mafundisho ya Neno la Mungu yaliyo wazi na kwa utaratibu. Imani yake thabiti na kujituma kwake katika kujifunza Maandiko vilimfanya kuwa mmoja wa walimu waliopendwa na wanaoheshimika wa Biblia wa wakati wake.

Derek ni mwandishi wa vitabu zaidi ya 100 na kuacha hazina kubwa ya thamani ya nyenzo za mafundisho ya Biblia ambavyo ni alama ya maisha na kazi aliyoifanya kwa dhati alipokuwa hai. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha zaidi ya 100, na kubaki kama hazina ya kuchochea na kujifunza kwa mamilioni ya Wakristo ulimwenguni mwote.

Mwaka mmoja kabla ya kufariki kwake mnamo 2003, mwandishi wa habari wa The Jerusalem Post alimwuliza je ni nini mahitaji makubwa ya Kanisa leo. "Walimu wa Biblia" alijibu Derek. "Walimu makini wa Biblia." Mwandishi huyo akikumbuka mahojiano hayo, mnamo mwaka 2006 aliandika: " Hakika, wamekuwepo wachache kama yeye."

Huduma ya Derek Prince

Mnamo mwaka 1971, Derek alifungua rasmi ofisi huko Fort Lauderdale, Florida, ili kuchapisha na kusambaza mafundisho. Mwanzoni ilijulikana kama Derek Prince Publications, huduma ilipanuka na ilipofika mwaka 1990 ilipewa jina la Derek Prince Ministries (Huduma ya Derek Prince).

Leo, Huduma ya Derek Prince ina ofisi katika nchi zaidi ya 45 duniani zikiwemo Australia, Kanada, China, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, New Zealand, Norway, Urusi, Afrika Kusini, Uswizi, Uingereza na Marekani. Imeendelea kuwa na bidii ile ile ya kuwahudumia wenye njaa ya kiroho, na kwa kufanya hivyo, kudumisha maono ya Derek aliyotoa mnamo Julai 2002.

Ni shauku yangu, na pia naamini ya Bwana, kwamba huduma hii iendelee na kazi aliyoanzisha Mungu kupitia mimi kwa zaidi ya miaka sitini iliyopita, hadi Yesu atakaporudi.
Derek Prince